Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu watu wa nne kutumikia kifungo cha
mika 30 jela na kuchapwa viboko 12, sita wakati wa kuingia na sita
wakati wa kutoka baada ya kupatikana na hatia dhidi ya kosa la wizi wa
kutumia silaha.
Hukumu
hiyo iliyosomwa na hakimu Mkazi, Respicious Mwijage imewataja
waliofungwa kuwa ni Donald Nzweka, Michael Pascal,Ally Akili na Kurwa
Mwakagenda.
Akisoma
hukumu hiyo jana, Hakimu Mwijage alisema, upande wa mashtaka umeweza
kuthibitisha kosa hilo pasipo kuacha shaka na kuwa washtakiwa
walishiriki kutenda kosa na kwamba mahakama ilijiuliza kwamba kosa la
kutumia silaha ili lithibitike Jamhuri wana wajibu wa kuthibitisha bila
kuacha shaka kwamba mshtakiwa kabla ya kutenda awe na kifaa hatari au
wawe zaidi ya mmoja na kwamba baada ya tukio hilo walitumia nguvu kwa
mtu waliyepora.
Katika
kesi hii, mlalamikaji na mashahidi wengine walieleza kuwa usiku wa
julai 7 majambazi walivunja mlango mkuu wa nyumba yao kwa kutumia bomu
ambalo lilitambuliwa na polisi kuwa baruti na kisha kuendelea kuvunja
milango mingine ambapo baada ya hapo waliingia katika chumba walichokuwa
wamekaa, ambacho kilikuwa na mwanga, mshtakiwa mmoja alishika panga na
kuanza kuwapiga kwa kutumia ubapa.
Alisema,
kwa kuzingatia ushahidi huo hakuna shaka kwamba mashahidi waliweza
kuwatambua majambazi na kuwa utetezi wa washtakiwa kwamba walikamatwa
maeneo tofauti na kupelekwa oysterbay polisi na kupigwa na kunyanyaswa
siyo ya kweli.
Kabla
ya kusomwa kwa adhabu hiyo, Hakimu Mwijage aliuliza upande wa mashtaka
kama walikuwa na lolote na kusema juu ya washtakiwa ambapo wakili wa
serikali Gloria Mwenda, alidai washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza
na akaomba wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa jamii.
“Nimeridhika
ushahidi wa mashahidi 11 walioletwa na upande wa mashtaka ambao
wameweza kuthibitisha bila ya kuacha shaka kuwa mlitenda kosa,
nawahukumu kwenda jela miaka 30 na kuchapwa viboko 12, sita siku
mnaingia na sita siku ya kutoka" alisema Mwijage.
Awali
ilidaiwa, Julai 7 ,2013 huko maeneo ya Boko Magengeni, jijini Dar es
Salaam, washtakiwa hao waliiba simu nne pesa taslimu 150,000 na cheni
za dhababu mbili ambapo vitu vyote vina thamani ya 2, 050,000 mali ya
Hobokela Mwakijambile.
No comments:
Post a Comment