Agustino Steven (8) na Rebeka Steven(7) wakiwa nje ya nyumba wanayoishi
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida watoto wawili
wenye umri wa miaka saba na nane wametelekezwa na wazazi wao kwa muda wa miezi
matano bila huduma za msingi.
Watoto hao wamefahamika kwa majina ya
Agustino Steven (8) na Rebeka Steven(7) ambao ni wanafunzi wa darasa la
kwanza shule ya msingi Mapambano
iliyopo Kata ya Iyela Jijini Mbeya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watoto
hao wamesema Wazazi wao waliwaacha kwenye nyumba ya kupanga tangu mwezi wa Mei
mwaka huu ambapo Baba inasadikika alielekea Umalila Mbeya Vijijini ambako
inasemekana ameoa mke mwingine.
Wamesema Mama yao alielekea Mbozi ambako
pia naye inasadikika ameolewa na mwanaume mwingine hivyo kuwaacha watoto bila
kuwa na huduma za msingi kama Chakula na mavazi huku wakiwa wameachiwa Nyumba mtaa wa Jakaranda Airport.
Aidha watoto hao waligundulika baada ya
kukutwa mitaani wakitafuta riziki kwa kuzoa taka kwenye majumba ya watu kisha
kupeleka majalalani kwa ujira wa kati ya shilingi 200 na 500 ambazo huzitumia kununua mahitaji ya
nyumbani pamoja na kujipikia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Dawati la Jinsia chini ya Jeshi la
Polisi, Mary Gumbo amesema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio
na kuwahoji watoto hao ambapo pia aliwaomba majirani na wananchi kulisaidia
jeshi la Polisi ili kuwabaini wazazi walipo ili wachukuliwe hatua kali za
kisheria.
Amesema majirani pia waendelee kuwa
karibu na watoto hao hadi pale wazazi wao watakapopatikana kwa kuwahudumia na
kuhakikisha wanaendelea na masomo kama kawaida.
Amesema kitendo kilichofanywa na wazazi
hao ni cha kinyama hivyo wakipatikana hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ambapo
pia alitoa wito kwa jamii kuacha vitendo vya kikatili.
|
No comments:
Post a Comment