Saturday, 12 October 2013

Mwalimu Nyerere alianza safari ya maisha Magomeni

magomeni_d8c90.jpg
Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo eneo la Magomeni ambayo kwa sasa ni makumbusho ya Taifa
Wakati Taifa linaadhimisha miaka 13 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, pia anakumbukwa kwa namna alivyoona umuhimu wa kununua kiwanja na kujenga nyumba yake mwenyewe, eneo la Magomeni mkoani Dar es Salaam.
Enzi hizo Magomeni ndiyo ilikuwa kama Masaki. Mwalimu Nyerere alimwomba rafiki yake Mustafa Songambele amtafutie kiwanja katika maeneo hayo, naye akampatia hicho ambacho sasa ipo nyumba ambayo imegeuzwa Makumbusho ya Taifa.
Mhifadhi Malikale anayesimamia nyumba hiyo, Emmanuel Katoroki anasema si serikali iliyoamua kuifanya nyumba hii kuwa makumbusho bali Mwalimu Nyerere mwenyewe, ambaye alitaka Watanzania wajue ilipotoka historia yake kisiasa.(P.T)
Katoroki anasimulia kuwa Mwalimu Nyerere baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu, alitafuta sehemu ya usalama na ndipo rafiki yake alipomtafutia kiwanja hicho kilichopo Magomeni, Mtaa wa Ifunda.
"Mwalimu alikinunua kiwanja hiki mwaka 1957. Hii ilikuwa ni baada ya kupata tetesi kuwa anaweza kuwa Waziri Mkuu na wakati ule alihitaji ulinzi kwa kuishi katika mazingira salama, kwa kuwa Magomeni enzi zile ndiyo ilikuwa kama Masaki sasa hivi, akanunua na kuanza ujenzi," anasema Katoroki.
Ulinzi wake
Katoroki anasema kwa wakati ule ulinzi ulikuwa mdogo hivyo kwa mtu anayeanza kuchipukia kisiasa tena anayetajwa kuweza kushika nafasi kubwa katika nchi, alihitaji kujilinda kwa kuwa lolote lingeweza kutokea.
Aidha, Katoroki anasema historia ya kisiasa ya Mwalimu ilianza wakati akiishi katika nyumba hii na baada ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwani baada ya hapo alikwenda kuishi katika nyumba ya serikali Sea View na baadaye Ikulu.
"Pia ni nyumba ya kihistoria kwani aliijenga kwa kiinua mgongo chake baada ya kuacha ualimu pale Shule ya Sekondari ya Pugu. Baada ya kuwepo tetesi na pengine mwenyewe alikuwa na taarifa kamili, aliamua kuachana na ualimu, " anasema Katoroki.
"Ninasema historia yake kisiasa ilianzia katika nyumba hii kwani aliamkia katika nyumba hii kwenda kuapishwa kuwa Waziri Mkuu na kuanza rasmi shughuli za kisiasa na ukombozi wa bara la Afrika," anasema.
Kingine ambacho kinaifanya nyumba hii kuwa ya kihistoria ni pamoja na kuwa alijinyima wakati akijenga, aliishi kwa muda wa miezi minane tu kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika Januari 1, 1960.
Katoroki anasema pamoja na nyumba hiyo kuwa ya pekee, Mwalimu aliwahi kuiuza baada ya kutokea mgogoro katika familia yake iliyokuwa ikiiogombea.
"Inavyoonekana Mwalimu baada ya kuwa Waziri Mkuu aliitelekeza nyumba hii na ndugu wakaanza kuigombania. Mwenyewe baada ya kupata taarifa hizo aliamua kuumaliza ugomvi wa ndugu kwa kuiuza," anasema Katoroki.
Hata hivyo historia nyingine iliandikwa mwaka 1973 wakati Jumuiya ya Wafanyakazi (JUWATA), ikitimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake ambayo Mwalimu Nyerere alialikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na Jumuiya hiyo iliamzawadia nyumba.
"Juwata walimwambia Mwalimu tunataka kukupa zawadi, alipoifungua alikuta ni hati ya nyumba yake ambayo aliwahi kumuuzia mtu mwingine," anasema Katoroki.
Viongozi wa Juwata walimnunulia Mwalimu Nyumba hiyo kutoka kwa mtu aliyemuuzia kwa Sh 35,000 na kumrudishia mwenyewe kwa njia ya zawadi.
Aliwashukuru kwa kuirudisha mikononi mwake. Hata hivyo alisema asingependa ibaki kwenye mikono yake kwani inaweza kurudisha matatizo aliyoyakwepa na hivyo akaamua kuitoa kwa serikali ili iifanye kuwa Nyumba ya Makumbusho.
Serikali kwa muda mrefu iliitelekeza nyumba hii na hivyo kuanza kuharibika na vyombo kuanza kupotea. Hata hivyo, Wizara ya Utamaduni ilipewa jukumu la kuisimamia nyumba hii chini ya Idara ya Mambo ya Kale na mwaka 2002 ilikabidhiwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Idara ya Mambo ya Kale.
Vitu vyake
Pamoja na kuwa vitu vingi vya Mwalimu vilipotea baada ya Mwalimu Nyerere na familia yake, ndani ya nyumba hiyo vipo vitanda vya familia kikiwamo kile alichokilalia mwalimu mwenyewe kabla ya kuhama.
Vitu vingine vilivyopo ni kabati la jikoni, kabati la kuhifadhia fedha (kibubu), pasi ya mkaa, mtungi wa kuhifadhia maji, redio ya mbao, makochi, cherehani na vyombo vya jikoni.
Pamoja na vyombo ndani ya nyumba hiyo, kuna noti za pesa zilizokuwa zikitumika enzi za utawala wake. Pia vipo vitabu alivyowahi kuandika kama vile; Ujamaa ni Imani, Maendeleo ni Kazi, 'Education to Self Relience', Tujisahihishe, Tanu na Raia, 'Our Leadership and Destiny of Tanzania' na vingine vingi.
Vitu vingi vilivyopo ndani ya nyumba hiyo vilipatikana kutoka kwa Mzee Omary (Aliyekuwa baba mlezi wa Mwalimu Nyerere), ambaye inadaiwa kuwa baada ya kuona nyumba haina mwelekeo alivichukua na kwenda navyo Dodoma ambako anaishi mpaka sasa.
"Mzee huyu ametunza vitu vingi vya Mwalimu na kama unavyoona humu ndani, hivi vyote tumevipata kwake, tunasikia kuna vingine walichukua ndugu na sasa wameviuza kwa watu wa makumbusho binafsi," anasema Katoroki.
"Nia yetu ni kupata kila kitu ambacho kilikuwamo humu ndani, vingi viliuzwa kwenye makumbusho binafsi na wao wanaviuza kwa bei za juu hivyo si rahisi kuvipata," anasema Katoroki.
Chanzo:Mwananchi

No comments: