MTOTO wa
kike mwenye umri wa miaka tisa ameonesha ujasiri wa kipekee kwa kumwokoa
mama yake mzazi, Magreth Ibrahim (50) kuuawa na mamba baada ya
kupambana na mnyama huyo kwa zaidi ya nusu saa.
Mama huyo
mkazi wa kijiji cha Karema, mwambao mwa Ziwa Tanganyika wilayani
Mpanda, kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Mpanda mjini
Mpanda kwa matibabu baada ya mkono wake kunyofolewa na mamba
aliyemshambulia wakati akifua kando ya Mto Ikola.
Akimweleza
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima aliyemtembelea hospitalini hapo
masaibu yaliyomsibu, alisema anamshukuru sana binti yake mwenye umri wa
miaka tisa aliyeweza kuokoa maisha yake licha ya kuwa amenyofolewa
mkono na mamba huyo.
Akisimulia
mkasa huo, Magreth alieleza kuwa juzi akiwa anafua kando ya mto Ikola
ghafla mnyama huyo aliibuka majini na kumpiga usoni na mkia wake.
"Mamba
huyo aliibuka ghafla mtoni na kunichapa usoni na mkia wake nami
nikaangukia majini ndipo aliponidaka mkono wangu na kunivutia mtoni
....binti yangu aliyekuwa jirani yangu alipoona niko karibu kuliwa na
mamba kwa ujasiri aliweza kukabiliana naye ... Alinishika mkono mwingine
na kunivutia nje huku akipiga kelele kumtisha mnyama huyo ili aniachie
hatimaye akaunyofoa mkono wangu na kutokomea nao mtoni ...." alieleza.
Aliongeza
kuwa watu waliokuwa wakifua mtoni hapo wengi wao wakiwa wanawake
walifika eneo la tukio ambapo wakiwa na binti yangu walimvuta na kumtoa
nje na baadae wakamkimbiza hospitalini mjini Mpanda kwa matibabu.
Naye
Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Mkemwa amethibitisha
kuwa hali ya mama huyo inaendelea kuimarika baada ya kupatiwa matibabu. (HABARI LEO)
No comments:
Post a Comment