Saturday 2 May 2015

Rais Kikwete Awajibu Walimu Waliomhoji Kwa Bango Anawaachaje.....Aahidi Kuwalipa Madai Yao Kabla Ya Kung'atuka




RAIS Jakaya Kikwete amewajibu walimu kuwa katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wake amefanya kazi ya uboreshaji maslahi yao na kuahidi kumaliza madai yao yote kabla hajang’atuka madarakani Oktoba mwaka huu.
 
Kikwete alisema hayo alipokuwa akiwajibu walimu ambao waliandika bango kwenye maandamano ya sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani na kupita mbele yake na kusomeka kuwa ‘Shemeji Unatuachaje?’ ikiwa ni lugha ya utani kwa kuwa mke wake Mama Salma ni mwalimu.
 
Maandamano hayo yalifanyika katika Jiji la Mwanza ambapo Kikwete alikuwa mgeni rasmi. Katika majibu yake alisema ameboresha miundo ya utumishi katika sekta mbili za walimu na afya.
 
Aliwaambia walimu mambo aliyoyafanya ni kuanzishwa kwa Muswada wa Bodi ya taaluma ya walimu na Tume ya utumishi ya walimu lengo ni kuwasaidia, kuwainua pamoja, kuwaendeleza na kufanya kila kitu katika sekta hiyo.
 
Alisema maandalizi yake yameshakamilika bado kupelekwa bungeni. Alisema Bodi ya taaluma ya walimu itawaendeleza walimu kitaaluma.
 
Katika hotuba hiyo kwa wafanyakazi iliyotumia zaidi ya saa moja, Kikwete alisema anatumia nafasi hiyo kuwaaga ‘shemeji’ zake ambao ni walimu, kwani imebakiza muda mfupi amalize muda wake.
 
Alisema muundo wa walimu umeanza Julai mwaka jana wa kulipa malimbikizo yao lakini haukuenea katika maeneo yote kwa haraka, lakini mwaka mpya wa fedha jambo hilo litawekwa vizuri.
 
Alisema malimbikizo ya walimu 30,668 hivi sasa ni Sh 53,155,440,406 na walimu 29,143 wamelipwa Sh bil 25.223 huku madai ya walimu 7,668 ambayo ni Sh bilioni 9.2 yatalipwa mwaka mpya wa fedha.
 
Lakini baadhi ya madai hayo ya walimu 30,807 ya Sh bilioni 17.3 yamekutwa na dosari mbalimbali na kutaka yarudishwe ili halmashauri iyahakiki na yalipwe.
 
“Fanyeni hima dosari zikamilike walipwe. Baada ya kusema hayo nina uhakika ninawaacha vizuri,” alisema Rais Kikwete.
  
Pia alielezea furaha yake ya uanzishwaji wa benki ya walimu, ambayo serikali inaiunga mkono na kutoa ushirikiano ili lengo la walimu litimie.
 
Akizungumzia kada ya uuguzi, Rais Kikwete alisema serikali ilibadilisha muundo mwaka 2010 ambao uliathiri baadhi ya wauguzi kwa kuwa viwango vyao vya mishahara vilishuka, hilo ni kosa.
 
“Nimeagiza warejeshewe mishahara yao ya awali na malimbikizo yalipwe,” alisema. Alisema katika kada hiyo mwaka 2010 watumishi 476,430 walipandishwa vyeo.

No comments: