Rais Jakaya Kikwete
JUMUIYA
ya Kimataifa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini hapa,
imeelezea msimamo wake thabiti wa kuunga mkono kwa dhati na kwa kila
hali kazi na jukumu ya Jopo la Watu Mashuhuri Duniani la Kukabiliana na
Majanga Duniani linaloongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Jumuiya
hiyo imeeleza msimamo wake wa kuunga mkono Jopo hilo wakati Rais Kikwete
na wana-Jopo wenzake walipopata nafasi ya kuwaelezea Wawakilishi wa
Kudumu wa nchi mbali mbali duniani katika Umoja wa Mataifa kuhusu kazi
iliyofanywa na Jopo hilo katika siku za mwanzo kabisa.
Jopo hilo
lililotangazwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon
Aprili 2, mwaka huu, limepewa jukumu ya kupendekeza jinsi gani dunia
inavyoweza kukabiliana na majanga ya kiafya duniani, na hasa magonjwa ya
milipuko, kama ilivyokuwa ebola katika nchi za Afrika Magharibi za
Guinea, Liberia bna Sierra Leone.
Baada ya
wiki moja ya kazi kubwa mjini New York, Rais Kikwete na wajumbe wa Jopo
hilo kutoka Brazil, Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, walikutana
na Wawakilishi wa Kudumu wa mataifa mbali mbali katika UN kuwaelezea
nini kimefanyika na nini kinatarajia kufanyika.
Baada ya
maelezo ya wajumbe wa Jopo, mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani katika UN
alisema kuwa Ujerumani inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo
akisisitiza kuwa Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel amekubali kutoa
kiasi cha dola za Marekani milioni moja (sh bilioni 1.9) kuunga mkono
shughuli za Jopo hilo.
Mwakilishi
wa Senegal alisema kuwa nchi yake inaunga mkono moja kwa moja kazi ya
Jopo hilo lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN, akisisitiza kuwa Senegal,
kama Mwenyekiti wa Kamati ya Oslo ya Afya katika Umoja wa Mataifa
itashirikiana na Jopo hilo moja kwa moja.
Mwakilishi
wa Ufaransa alisema kuwa nchi yake inaunga mkono kazi ya Jopo moja kwa
moja na kuwa ni uamuzi wa busara wa Katibu Mkuu wa UN kuunda Jopo hilo.
Mwakilishi
wa Uingereza alipokea kwa mikono miwili uundwaji wa Jopo hilo,
akisisitiza kuwa nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Jopo hilo
kama ilivyoiunga mkono Sierra Leone wakati wa kukabiliana na ebola.
Mwakilishi
wa Luxembourg alisema kuwa dunia inalitarajia Jopo hilo kuelekeza nguvu
yake katika mapendekezo ya uongozi kuliko changamoto za kiufundi.
Aidha,
ameongeza kuwa nchi hiyo baada ya kushika Uenyekiti wa Umoja wa Ulaya
(EU) itaongeza kazi yake katika kuchunguza athari za ebola na kiini
chake.CHANZO: HABARI LEO
No comments:
Post a Comment