LICHA ya
Chama cha Wananchi (CUF) kudai mara kwa mara kuwa kilishinda uchaguzi wa
Urais mwaka 2010 visiwani Zanzibar, Katibu Mkuu wake Maalim Seif Sharif
Hamad, amekiri kuwa hawana ushahidi stahiki wa kuthibitisha ushindi
huo.
Kiongozi
huyo ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, amekiri wazi kuwa
na nia ya kuwania nafasi ya Urais visiwani humo katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu na kusisitiza kuwa ataeleza sababu na maandalizi yake ya nia
hiyo hivi karibuni.
Maalim
Seif aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu maandalizi ya uandikishwaji wapiga kura wapya visiwani
humo katika daftari la wapiga kura, unaotarajiwa kuanza rasmi Mei 16
hadi Juni 25, mwaka huu.
"Uchaguzi
wa mwaka 2010 ulifanyika mara baada ya Wazanzibari kuamua tuwe na
maridhiano, hivyo uchaguzi ule kwa kiasi kikubwa ulikuwa huru na wa
amani na katika kampeni hakuna hata nzi aliyebanwa," alisema Maalim
seif.
Alisema
baada ya kupiga kura katika uchaguzi huo, muasisi mmoja wa maridhiano
hayo ambaye wakati huo alikuwa bado Rais wa Zanzibar, Amani Abeid
Karume, alimtumia mjumbe ambaye alimsisitizia juu ya umuhimu wa
kuzingatia maridhiano yaliyopo na maslahi ya nchi hasa amani.
Alisema
kwa mujibu wa mzee huyo aliyetumwa na Rais Karume, alimtaka Maalim Seif
na CUF kwa ujumla pindi matokeo yatakapotoka kutoendeleza mvutano.
"Hata
hivyo hakukua na haja ya mvutano kwani Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
ilipotangaza matokeo, tuliwasilisha hoja yetu kuwa tumeshinda, tume
ikatutaka tuwasilishe (result slip) nakala za matokeo ili kuthibitisha
madai yetu," alisema.
Hata
hivyo, alisema chama hicho kilishindwa kuwasilisha nakala zote za
matokeo na hivyo kukosa ushahidi kutokana na baadhi ya mawakala wa chama
hicho kuwaangusha kwa kukosa nakala hizo.
"Hivyo
hiyo hoja kwamba nishauriwa nimuachia ushindi Rais wa Zanzibar Dk Ali
Mohamed Shein, haikuwa na sababu kwa kuwa hatukuwa na ushahidi wa
kuniwezesha kuthibitisha ushindi wangu," alisisitiza.
Alisema
katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu, chama hicho
kimejipanga na kuhakikisha kinakuwa na mawakala waaminifu na na
watendaji.
Maalim
Seif alianza kugombea urais visiwani Zanzibar kwa mara ya kwanza mwaka
1995 baada mfumo wa vyama vya vingi kurejeshwa rasmi, lakini alishindwa.
Aligombea nafasi hiyo tena mwaka 2000, 2005 na 2010, ambako kote alishindwa na nafasi hiyo kuchukuliwa na CCM.
Awali,
akizungumzia maandalizi ya uandikishaji wapiga kura katika daftari la
kudumu, kiongozi huyo aliitaka ZEC kuhakikisha, inahakiki kwanza daftari
la wapigakura la mwaka 2010 na kuondoa majina ya wale wote wasiostahili
na kuandikisha wapigakura wapya wanaostahili.
"Katika
utafiti tulioufanya chini ya kitengo cha Sera, Utafiti na Mafunzo cha
CUF kupitia daftari la kudumu la wapigakura la mwaka 2010 na 2013,
tulibaini takribani wapiga kura 10,000 waliandikishwa isivyostahili,"
alisema.
Alisema
anaamini kuwa kasoro zote zilizojitokeza katika daftari hilo na uchaguzi
kwa ujumla, zinaweza kufanyiwa kazi na Tanzania ikafanya uchaguzi wake
kwa amani na kuwa mfano barani Afrika.
Alionya
dhidi ya vitendo vya ubabe, vurugu na hadaa za baadhi ya vyama kwa ajili
ya kujihakikishia ushindi kuwa ni chanzo kikubwa cha kuvurugika kwa
amani kama ilibyotokea Zanzibar mwaka 2005 jambo ambalo linahitaji
kukemewa.
"Lazima
tutambue kuwa kila mtanzania ana haki ya kugombea na kuchaguliwa, ni
vyema sote tukakubali kuwa hakuna mwenye hati miliki na haki ya nchi hii
pekee. Tuheshimu matakwa ya wananchi," alisema.
Alisema
ili kuepusha nchi na vurugu wapigakura wote haramu waliopatiwa
vitambulisho vya uzanzibari kinyume na Sheria wanyang'anywe vitambulisho
hivyo na watu wote wenye haki ya kupatiwa vitambulisho vya ukaazi
Zanzibar wapewe kabla tarehe ya uandikishwaji haijaanza.
Aidha,
alivitaka vikosi vya ulinzi na sualama ikiwemo Jeshi la Ulinzi la
Wananchi (JWTZ) na Idara Maalum Zanzibar, viache kutumiwa kisiasa na
kwenda kinyume na Sheria zinazoongoza kazi zao, idara zote za usajili
ikiwemo ZEC nazo zijiepushe kutumika kisiasa ikiwemo Jeshi la Polisi.CHANZO: HABARI LEO (Muro)
No comments:
Post a Comment