Wednesday, 20 April 2016

Kauli ya Mkurugenzi wa Jiji La Dar es Salaam Wilsoni Kabwe Baada ya Kutumbuliwa Jipu Darajani na Rais Magufuli


Mkurugenzi  wa Jiji la Dar es Salaam aliyesimamishwa kazi, Wilson Kabwe amesema hahusiki na tuhuma zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Kabwe alitoa kauli hiyo, baada ya kutafutwa na mwandishi wetu ili kupata maoni yake baada ya Rais Dk. John Magufuli kutangaza kumsimamisha kazi.

Mwandishi: Habari mkurugenzi?

Kabwe: Salama.

Mwandishi: Tumepata taarifa za kusimamishwa kwako kazi na Rais kutokana na tuhuma zilizotolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makonda tunaomba maoni yako. 

Kabwe: Sijasikia ndiyo kwanza unaniambia wewe, kasema lini Rais?

Mwandishi:Leo wakati akizindua Daraja la Kigamboni.  
Kabwe: Alitamka palepale au?

Mwandishi: Ndiyo.Nataka kujua unazungumziaje uamuzi huo?

Kabwe alisema tuhuma zinazoelekezwa kwake ni za uongo na kwamba zimelenga kumchafua mbele ya Rais Magufuli.

Mkurugenzi huyo alishangaa kuhusishwa na tuhuma hizo na kusema kuwa, wakati sheria ndogo zinapitishwa na uongozi wa Jiji la Da es salaam yeye hakuwa Mkurugenzi wa Jiji hilo.

“Sihusiki na mikataba inayosemwa, huu ni uongo mtupu, Makonda ametoa taarifa za uongo kwa Rais.

“Tuhuma zinazoelekezwa kwangu ni za uongo na zimelenga kunichafua mbele ya Rais, nasisitiza tena hakuna mkataba wowote ambao ofisi yangu iliingia kwa nia ya kupoteza mapato ya Serikali,” alisema Kabwe huku akihoji kuwa ikibainika hahusiki atalipwa fidia?

Kuhusu Kustaafu Kazi

Alisema kutokana na hali ya afya kutokuwa nzuri, Desemba mwaka jana aliomba kustaafu utumishi wa umma na kuandika barua kwa Rais ili aendelee na matibabu.

Alisema tangu aandike barua hiyo, hajawahi kujibiwa na kusisitiza kuwa anamheshimu Rais Magufuli na anaamini atatenda haki baada ya vyombo husika kufanya uchunguzi juu ya tuhuma hizo.

No comments: