Thursday 20 July 2017

Tundu Lissu Jana Alitoa Kali........Ni Baada ya Kugoma Kutoka Mahakamani Akihofia Kukamatwa na Polisi


SeeBait
Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu  jana  aligoma kutoka katika chumba cha mahakama kufuatia kuwepo kwa tetesi kuwa kuna baadhi ya polisi wametumwa kumkamata kiongozi huyo. .

Lissu alifika mahakamani hapo jana asubuhi kwa ajili kusimamia kesi ya migogoro ya ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) iliyokuwa ikisikilizwa na Hakimu Proches Mushi.

Katika kesi hiyo, Kamati ya Utendaji ya CWT wilaya imefungua kesi dhidi ya Katibu Mkuu wa CWT, Yahaya Msulwa wakimtuhumu kwa matumizi mabaya madaraka.

Hata hivyo wakijadili muda wa kurudi tena kwa kesi hiyo, Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS) alisema kuna polisi waliovalia kiraia waliokuwa wakimngojea nje ili wamkamate na kumsafirisha kwenda Dar es Salaam.

Habari za kutaka kukamatwa kwa Lissu zilisikika  asubuhi katika mitandao ya kijamii baada ya kutumiwa ujumbe kuwa kuna maaskari waliovalia kiraia wanataka kumkamata.

“Mheshimiwa naomba kesi hii isisomwe tarehe 23 kwa sababu sitakuwepo nchini, natarajia kwenda Uganda kwenye kikao cha vyama vya Afrika Mashariki vya mawakili,”alisema na kuongeza:

“Lakini pia nimepewa taarifa kuwa hapo nje kuna polisi wananisubiri nikitoka wanikamate na kunisafirisha kwenda Dar es Salaam hivyo huenda tarehe hiyo (Julai 23) nisiwe huru kuhudhuria kesi.”

Akijibu maombi hayo Mushi alisogeza kesi hiyo hadi Septemba 27-29 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Mara baada ya kesi kuahirishwa, Lissu akafanya mkutano na waandishi wa habari ndani ya ukumbi wa mahakama hiyo na kudai hatatoka mahakamani hapo ili aone kama polisi wana uwezo wa kuingia na kumkamata.

“Leo asubuhi nimepata taarifa kutoka Dar es Salaam kwa mama watoto wangu kwamba polisi walikuja nyumbani kwangu kunitafuta na wakaelezwa kwamba yuko Dodoma kwa muda wa siku tatu,” alisema.

“Baada ya hapo wasamaria wema walinitaarifu kuwa Jeshi la Polisi Dar es Salaam limewaomba wenzao wa Dodoma wanikamate pindi tu nitakapotoka hapa na kunirejesha Dar es Salaam.”

Alipoulizwa sababu inayofanya polisi watake kumkamata, Lissu amesema ni kutokana na maoni yake aliyoongea juzi ya kuukosoa uongozi wa Rais Magufuli.

“Rais Magufuli na chama chake wameshindwa siasa na wanachofanya sasa ni kutumia mabavu lakini wao kama Chadema kamwe hawataogopa wala kukaa kimya kwani kazi yao si kumsifia Rais bali ni kumkosoa anapofanya vibaya,”amesema.

Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema hakuna sheria yoyote inayowaruhusu polisi kumkamata wakili akiwa katika shughuli zake mahakamani.

“Nakaa nione kama watavunja sheria ya kuja kunikamatia hapa hapa mahakamani. Nimeshazoea kukamatwa tangu mwaka huu uanze nimekamatwa mara nne,”alisema.

Baada ya kukaa mahakamani kwa saa nne, alifika Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa na kumweleza Lissu kwamba Jeshi la Polisi Dodoma halina taarifa yoyote wala mpango wowote wa kumkamata.

“Hatujapokea taarifa yoyote wala maelekezo yoyote ya kukukamata kutoka makao makuu. Hata ingekuwa hivyo tungeshakukamata kwa sababu muda wa mahakama umekwisha. Kwa sasa hivi yamebakia majengo tu kwa hiyo uwe huru uendelee na shughuli zako,” Mambosasa alimwambia mbunge huyo.

Baada ya Mambosasa kuondoka katika mahakama hiyo, Lissu naye aliondoka katika eneo hilo.

No comments: