Chadema
imesema haitabadili msimamo wake wa kutaka wataalamu kutoka nje
kuchunguza shambulio dhidi ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Juzi,
Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba alisema hakuna haja ya
kuhangaika kutafuta wachunguzi kutoka nje kwa kuwa mazingira
watakayofanyia kazi ni yaleyale na hivyo kuitaka Chadema kuviamini
vyombo vya ndani vya uchunguzi.
Lakini
jana, Chadema imeeleza kuwa haioni kinachoendelea na hata kama ni
mazingira yaleyale, wachunguzi kutoka nje ndiyo muafaka.
Lissu,
mmoja wa wabunge wa upinzani asiye na woga wa kusema anachokiamini,
alishambuliwa kwa risasi mchana wa Septemba 7 akiwa katika gari nje ya
makazi yake mjini Dodoma akitokea bungeni.
Pamoja
na washambuliaji kufyatua risasi zipatazo 32, Lissu alinusurika kifo na
kupelekwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na baadaye alipelekwa Nairobi,
Kenya kwa matibabu zaidi, safari ambayo iligubikwa na mabishano baina ya
Chadema, uongozi wa Bunge na Serikali, iliyotaka ahamishiwe Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Chadema
imekuwa ikihusisha shambulio hilo na tofauti za kisiasa na hivi
karibuni ilisema pamoja na kuwa na imani na vyombo vya usalama, inataka
wachunguzi kutoka nje kwa kuwa vyombo vya dola vimetuhumiwa.
Mkurugenzi
wa itikadi na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema jana kuwa
ikiwa Serikali haina hofu, iruhusu wachunguzi hao ili yapatikane majibu
ya nani alihusika.
Mrema alisema hakuna haja ya kuzuia wachunguzi hao kwa kuwa wana uwezo wa ziada.
“Kwa
nini Serikali haitaki wachunguzi huru? Ni kweli kwamba wakija watafanya
kazi kwa mujibu wa sheria za nchi, lakini hii haibadili msimamo wetu,
hawa wana vifaa na wanaweza kusaidia kupata majibu,” alisema Mrema.
Alisema
tangu kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto alipotoa
taarifa za awali za tukio hilo, hakuna taarifa nyingine zozote
zilizopatikana, jambo ambalo alisema linaendelea kuwatia hofu.
Mrema
alisema yapo mauaji mengi kama ya Kibiti ambayo wananchi hawajui
matokeo ya uchunguzi wala hakuna waliofikishwa mahakamani.
Kiongozi
huyo wa Chadema alisema hata suala la mauaji ya Kibiti halijatolewa
taarifa wala watuhumiwa kufikishwa mahakamani, huku kada wa chama hicho,
Ben Saanane akiwa hajulikani alipo na mauaji ya mwenyekiti wa Chadema
mkoani Geita, Alphonce Mawazo yakiwa hayajatolewa ripoti.
Alisema
wataalamu hao kutoka nje wapo tayari kuja kufanya kazi ya kuchunguza
tukio hilo na kwamba kitendo cha kuwakataa kinaongeza shaka kwao.
“Tunakaribia mwezi hatujui chochote,” alisema Mrema.
“Kwa hiyo muafaka ni wachunguzi huru. Mtu hawezi kupigwa risasi mchana kweupe tena Dodoma Mjini...” alisema.
Mbunge
wa Iringa Mjini, Peter Msigwa alisema kuzuia wachunguzi hao kunawafanya
wafikirie kuwa kuna watu ambao hawataki kuumbuka na kuongeza kuwa kama
nia ipo, iwaruhusu.
No comments:
Post a Comment