Thursday, 28 September 2017

Mwigulu Nchemba Aizungumzia Gari Iliyokuwa Ikimfatilia Tund Lissu Jijini Dar


SeeBait
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amesema gari ndogo ambayo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alidai lilikuwa likimfuatilia maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, iko Arusha na haijawahi kutumika Dar es Salaam.

Mwigulu amesema leo kuwa baada ya polisi kufuatilia gari hiyo wamegundua iliyokuwa inamfuatilia Lissu ilikuwa na namba batili huku gari halisi yenye namba hizo za usajili ikiwa Arusha.

“Utoaji wa taarifa na wenyewe haukuwa rasmi kwa mfano Lissu aliposema kuna gari inamfuatilia nilielekeza polisi wakaifuatilia ikakutwa Arusha kuna gari ndogo ya namba hizo kwa hiyo kuna moja iliweka namba batili.

“Ile gari ilikutwa kule kule na haikuwa na ruti ya huku (Dar es Salaam) huwa iko kule kule, kwa hiyo kwenye mambo haya ndiyo maana tunahitaji sana ushirikiano.

“Natamani watu hawa tungewatia nguvuni pale pale ningepewa ‘tip’ mapema tungefuatilia hili na  kitendawili cha watu wasiojulikana tungekitegua mara moja,” amesema Mwigulu akihojiwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds, leo.

Pamoja na mambo mengine amesema Lissu mwenyewe anaweza kusaidia uchunguzi katika tukio hilo ambapo pia ameonya watu watu wanaotengeneza matukio ya aina hiyo kufikiria madhara yanayoweza kutokea baada ya tukio.

No comments: