Jamii
ya Wahadzabe wanaojishughulisha na uwindaji, kurina asali na kukusanya
matunda porini, wameomba kupelekewa msaada wa bangi angalau tani mbili
watakayoitumia kwa mwaka mmoja.
Wahadzabe
wanaokadiriwa kufikia 500 ni jamii inayoishi porini maeneo ya
Endamaghan, Kandeni Tarafa ya Eyasi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.
Jamii hiyo, bado inakabiliwa na umasikini licha ya kuwa kivutio cha watalii katika Ziwa Eyasi.
Ombi
hilo walilitoa juzi katika Kijiji cha Endamaghan, wakati
walipotembelewa na timu ya wataalamu kutoka serikalini iliyoteuliwa
kuandaa mapendekezo ya muundo wa kipindi cha pili cha mpango wa kunusuru
kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Akizungumza
na Gazeti la Mtanzania katika eneo la makazi yao yenye nyumba za asili
za nyasi zilizoonekana kuwa wazi kutokana na kufunikiwa na nyasi
kidogo, Mwenyekiti wa jamii hiyo, Julius Ndaya alizitaja sababu alizodai
ni za msingi za kuomba wapelekewe bangi.
Alisema
shughuli za kutembea kutafuta wanyama kwa ajili ya kitoweo
huwalazimisha kutembea umbali mrefu kiasi cha kilomita 50, kazi ambayo
huwa ni sehemu ya majukumu ya mwanamume katika jamii hiyo.
“Kiasi
hiki cha tani mbili kinaweza kututosha watu kama 100 au 200 kwa miezi
6, tunavuta bangi si kama ambavyo wengine au Serikali wanafikiria kwamba
tunaweza kusababisha vurugu, kuvunja nyumba za watu, kuiba wala
kugombana na jamii nyingine, hapana.
“Mmea
huu tumeukuta babu zetu wakiwa wanauvuta wameturithisha, tunaendelea
kuvuta bila kuwa na madhara yoyote. Hii ni sehemu ya kiburudisho kwetu,
huku porini hatunywi pombe hii ndio pombe yetu. “Ikiwezekana turuhusiwe
kulima angalau bustani za bangi lakini changamoto kubwa tunayokutana
nayo ni pale Serikali inapopiga marufuku zao hili kwa madai kuwa ni
sehemu ya dawa za kulevya,” alisema Ndaya.
Kiongozi
wa jamii hiyo alikwenda mbali na kueleza pindi wanapovuta bangi
huchangamsha akili na miili yao, hivyo hujikuta wakipiga hadithi za
matukio ya uwindaji porini au namna walivyokabiliana na au kukurupushana
na wanyama wakati wa uwindaji.
Katika
eneo la jamii hiyo lenye nyumba za asili za nyasi zikiwa zimezungukwa
na mafuvu ya wanyama pori na miti mikubwa, lilikuwa na wanawake watu
wazima walionekana wamekaa kwenye makundi pamoja na vijana wa kiume
wakiendelea kuvuta bangi.
Akifafanua
kuhusu maombi ya Wahadzabe kuomba tani mbili za bangi, Mkuu wa Wilaya
ya Karatu, Theresia Mahongo alisema Serikali haiwezi kukubaliana na
maombi hayo.
“Hata
sasa walikuwa wakiniomba, majuzi tuliteketeza kiasi kama cha hekari
tano za bangi maeneo ya milimani, kwa hiyo kwa sasa hawaipati inawaumiza
zaidi.
“Kikubwa
tunaendelea kuwapatia elimu kwamba bangi kwao si kitu kizuri,
tutatafuta mbadala na kwa vile wameniomba nikutane nao hilo nalo
tutaliweka vizuri.
“Naamini
vipo vitu mbadala wanavyoweza kutumia badala ya bangi, mnawaona
wanalalamika kwa sababu hawaipati. Tunajua ni wawindaji wanakimbia na
kupita maeneo magumu ndio maana wanaihitaji ili iwatoe nishai, ukweli ni
kwamba jambo hilo hatuwezi kuliruhusu,” alisema.
Wakati
watu hao takribani 200 kutoka jamii ya Kihadzabe wakiomba kupelekewa
tani mbili za bangi, katika siku za hivi karibuni baadhi ya wabunge
waliomba zao hilo liruhusiwe kuwa la kibiashara ili kuwaongezea kipato
zaidi wakulima na wauzaji wa bangi.
Chakula
kikuu cha jamii hiyo ni mizizi, matunda pori, asali na nyama huku asali
ikiwa ni miongoni mwa vitu vinavyopendwa zaidi na jamii hiyo.
Namna
wanavyoitumia mizizi hiyo kwa chakula; wanakula kama ilivyo au kuichoma
na ladha yake ni kama muhogo au viazi na mizizi hiyo huwa na ukubwa
kama wa mguu wa mtu mzima.
Matunda
yao makuu ni kwantlanabe, kalahar, kongolobi na ubuyu ambayo husagwa
kwenye jiwe na unga wake husongwa kama ugali na kuchanganywa na asali.
Vyakula
vyao vinavyotegemea asili yao haviwapi fursa ya kutumia mafuta, nyanya,
kitunguu, sukari au kutumia vinywaji vya viwandani, isipokuwa chumvi.
Wanyama wanaopendwa zaidi na Wahadzabe ni pofu, nyani, tumbili, digidigi na twiga.
No comments:
Post a Comment