Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James ole Millya amemchongea kiongozi wa CCM kwa Rais John Magufuli, akisema amepora ardhi ya wananchi na akamuomba amchukulie hatua.
Bila kumtaja jina la kiongozi huyo, Ole Millya amesema, “Mheshimiwa Rais tunashukuru sana kwa kuja hapa na wewe umesema maendeleo hayana chama, naomba ushughulikie tatizo hili la wananchi kupokwa ardhi. Kuna mwenyekiti wa CCM amechukua ardhi ya wananchi na kujimilikisha sasa tunaomba uweke mkono wako ili tabia hii ikome.”
Ole Millya amesema hayo leo Jumatano alipowasalimia wananchi baada ya kupewa fursa hiyo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Barabara ya Kia - Mirerani yenye urefu wa kilomita 26.
Mbunge huyo pia amezungumzia kero ya ukosefu wa maji inayoendelea kuwakabili wananchi wa eneo hilo na akamwomba Rais awakumbuke wananchi.
Ole Millya amempongeza Rais kutokana na hatua yake ya kupigania rasilimali za umma na akataka hatua hiyo ianze kuwanufaisha wananchi wa Mirerani ambako yanapatikana madini ya Tanzanite.
“ Hapa kuna madini ambayo hayapatikani kwingine kokote isipokuwa ni hapa tu, lakini chakushangaza wananchi wamekuwa wakisafiri umbali mrefu hata kutumia malori kufuata maji, tunaomba msaada wako,” amesema.
Amesema anajua ni kwa nini Rais Magufuli wakati mwingine anakuwa na uchungu kutokana na upotevu wa rasilimali za umma.
“Tunaomba ubadilishe maisha ya wananchi hawa kwa kuwapatia maji safi na salama,” amesema.
No comments:
Post a Comment