Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa agizo kwa Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) kuhakikisha haitoi rufaa ya matibabu nje ya nchi ikiwa
wana uwezo wa kutibu maradhi husika hapa nchini.
Ummy amesisitiza wataalamu kutowaogopa wanasiasa
ikiwa wana uwezo wa kumtibu mgonjwa hapa nchini haina ulazima wa
kumwandikia rufaa nje ya nchi hata akiwa ni Rais John Magufuli.
Ametoa
agizo hilo leo Jumatatu wakati akipokea msaada wa vifaa vipya kwa ajili
ya vyumba viwili vya upasuaji vya watoto wadogo na wodi ya watoto ya
upasuaji vyenye thamani ya Dola za Marekani 675,000 sawa na Sh1.5
bilioni, kutoka kwa wataalamu na wahisani kutoka nchini Uingereza
kupitia taasisi ya Archie Wood Foundation.
"Rais
aliponiteua aliniagiza kwamba lazima niachane na rufaa za nje, hatuwezi
kuachana nazo ikiwa magonjwa yanayoweza kutibiwa ndani yatatibiwa nje,"
amesema Ummy.
Amesema Watanzania wana imani na
Muhimbili na hivi sasa wengi wanatoka hospitali za kulipia na kufuata
matibabu ila changamoto iliyopo ni majengo lakini wapo mbioni kujenga
jengo la ghorofa kwa ajili ya wagonjwa wa kulipia.
"Msitoe
rufaa ya mgonjwa kama hamjajiridhisha kwamba mnaweza kumtibu hapa hata
kama awe Rais, waziri au nani msitoe rufaa kwani maana yake mtakuwa
mmeshindwa ni lazima ninyi mseme kwamba hamuwezi na sisi
tutashughulikia," amesema.
Amewatahadharisha wataalamu
hao na wanasiasa kwamba lazima wahakikishe kweli hawawezi kutibu na
kwamba wizara ipo tayari na itawaunga mkono.
CHANZO ; Mwananchi
CHANZO ; Mwananchi
No comments:
Post a Comment