Tuesday, 12 September 2017

Waziri Mkuu Atoa Msaada Wa Sh. Milioni 10


SeeBait
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ametoa msaada wa sh. milioni 10 ili kumuwezesha Bw. Ernest Masenga kutatua changamoto zinazomkabili.

Bw. Masenga alikuwa msanii wa muziki wa dansi ambaye sasa anasumbuliwa na maradhi ya miguu. Pia makazi anayoishi si salama yanahitaji kukarabatiwa.

Waziri Mkuu ametoa msaada huo jana (Jumatatu, Septemba 11, 2017) katika makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar Es Salaam.

Ametoa msaada huo baada ya kuguswa na hali ya maisha ya msanii huyo aliyemuona kupitia kipindi maalumu kilichoonyeshwa na TBC Sempemba, 5, 2017. Kipindi hicho kiliongozwa na Bw. Godfrey Nago.

“Nawaomba Watanzania wenzangu tumsaidie mwezetu ili aweze kuishi vizuri kwa sababu sanaa yake imesaidia katika kuelimisha na kuburudisha umma .”

Kwa upande wake Bw. Nago ambaye amepokea msaada huo kwa niaba ya Bw. Masenga amesema atahakikisha anasimamia vizuri fedha hizo ili zitumike kama ilivyokusudiwa.

Pia Bw. Nago amesema anamshukuru Waziri Mkuu kwa kuwaunga mkono na kutoa msaada huo kwa sababu ameonesha kwamba Serikali inawajali wananchi wake na TBC itaendelea kuwaomba wadau mbalimbali wajitokeze na kumsaidia msanii huyo.

Naye Mjomba wa msanii huyo Bw. Kanuti Mloka ambaye ameiwakilisha familia amemshukuru Waziri Mkuu kwa msaada huo kwa kuwa familia imeshindwa kumsaidia Bw. Masenga kutokana hali duni ya maisha waliyonayo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 11, 2017.

No comments: