
Mtwara. Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon
Sirro amesema wanaendelea na upelelezi wa tukio la kushambuliwa na
kujeruhiwa kwa risasi Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu
Lissu.
IGP Sirro akizungumza leo Jumatano akiwa ziarani
mkoani Mtwara amemtaka dereva wa Lissu kulisaidia jeshi hilo katika
kukamilisha upelelezi.
Lissu ambaye anapata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya, alishambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Septemba 7 nyumbani kwake Area D mjini Dodoma na watu wasiojulikana.
Amesema
miongoni mwa wanaohitajika kwa kuhojiwa ni dereva wa Lissu ambaye
inaelezwa yuko Nairobi anakopatiwa matibabu ya kisaikolojia.
“Yule
kijana kwenye picha ukimwona yuko vizuri tu, sasa wanaposema anapata
huduma ya kisaikolojia wakati kwenye magazeti anaonekana hii inatupa
changamoto. Ndugu zangu, mheshimiwa Lissu amepigwa risasi na watu
tunaowatafuta, huyo kijana aje. Kuja kwake kutatusaidia kupata majibu ya
mambo mengi,” amesema IGP Sirro.
Amesema, “Mtu anasema anatibiwa kisaikolojia lakini kila siku nikiona magazeti anaonekana anawaka, inanipa tabu.”
IGP
Sirro amewataka waandishi wa habari kuwasilisha taarifa hiyo kwa umma
akisema, “Kimsingi waandishi wa habari naomba mlipeleke hili sisi tuna
uchungu sana na mheshimiwa Tundu Lissu, tunamheshimu ni mtu muhimu kwa
Watanzania na sisi tunataka tuwapate waliofanya lile tukio lakini
ushirikiano ni mzuri ili kufanikiwa,” amesema.
No comments:
Post a Comment