Wednesday 11 October 2017

MWAMUZI WA MBEYA CITY AONDOLEWA LIGI KUU YA VODACOM


Kamati ya Bodi ya Ligi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemuondoa Mwamuzi Msaidizi Grace Wamara kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa kukosa umakini na kutomsaidia Mwamuzi, hivyo kusababisha akubali bao lenye utata la Stand United dhidi ya Mbeya City.
Wamara alikuwa Mwamuzi Msaidizi Namba Mbili kwenye mechi hiyo namba 31 iliyofanyika Septemba 24 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga na wenyeji Stand United kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Uamuzi wa kumuondoa Wamara ambaye amerejeshwa katika Kamati ya Waamuzi ya TFF kwa ajili ya hatua nyingine umefanywa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(5) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
Klabu ya Stand United imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na wachezaji wake kuvaa jezi zenye namba tofauti na zile zilizosajiliwa. Wachezaji hao walivaa namba tofauti kwenye mechi namba 40 dhidi ya Simba iliyofanyika Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.
Stand United ilikiuka Kanuni ya 60(11) ya Ligi Kuu inayelekeza kuwa kila mchezaji atatumia namba ya kudumu ya jezi iliyosajiliwa na klabu yake wakati wa maombi ya usajili. Adhabu dhidi ya Stand United ni uzingativu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu.

No comments: