Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi itajumuika na Ulimwengu wote kuadhimisha Siku ya
Makazi Duniani, tarehe 02 Oktoba, 2017 – Karimjee Hall, ambapo Wadau
mbalimbali wanategemewa kujumuika katika hafla hiyo, itakayoambatana na
Maonyesho.
Siku ya Makazi Duniani
huadhimishwa duniani kote kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba. Lengo
kuu la maadhimisho haya ni kutoa mwongozo kwa nchi wanachama wa Umoja
wa Mataifa kutafakari kwa pamoja masuala yanayohusu makazi ulimwenguni
kwa kuangalia changamoto mbalimbali zilizopo na kushirikishana mbinu na
mikakati ya kupambana nazo.
Shirika la Umoja wa Mataifa
linalosimamia Makazi Duniani – UN-HABITAT hutoa mwongozo kupitia kauli
mbiu ambayo huongoza tafakari hiyo duniani kote. Mwaka huu maadhimisho
hayo, ambayo ni ya 32 yanafanyika kwa kuongozwa na Kauli Mbiu isemayo “Housing Policies”: Affordable Homes: Tafsiri ya kauli mbiu hiyo ni “Sera za Nyumba: Nyumba za Gharama Nafuu:
Kauli mbiu hii inaelekeza kutafakari namna tunavyoweza kutunga Sera za
Nyumba katika nchi zetu zinazojielekeza kutatua changamoto ya
upatikanaji wa nyumba, hususan za gharama nafuu ili kuwawezesha wananchi
wa kipato cha chini waweze kumudu kujenga, kununua ama kupanga.
Madhumuni ya Maadhimisho ya Siku
ya Makazi kufuatana na kauli mbiu ya mwaka huu Oktoba, 2017 ni
kuhakikisha kuwa Sera zetu za Nyumba na Makazi zinazingatia yafuatayo:
- Kuwa na Nyumba na Makazi bora yenye huduma za msingi za jamii toshelezi (Inclusive housing and social services),
- Kuwa na mazingira salama ya kuishi kwa wananchi wote, hususan wenye mahitaji maalum wakiwemo watoto, vijana, wanawake, wazee na wenye ulemavu (A safe and healthy living environment for all — with particular consideration for children, youth, women, elderly and disabled),
- Upatikanaji wa usafiri na nishati endelevu zenye gharama nafuu (Affordable and sustainable transport and energy),
- Kukuza, kulinda na kuhifadhi maeneo ya wazi mijini (Promotion, protection, and restoration of green urban spaces),
- Upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa na mfumo thabiti wa uondoshaji majitaka (Safe and clean drinking water and sanitation),
- Uwepo wa hewa safi na ya kutosha (Healthy air quality),
- Kuwepo fursa za ajira (Job creation) ,
- Kuimarisha upangaji miji na kuboresha makazi duni (Improved urban planning and slum upgrading),
- Kuwepo na mfumo thabiti wa usimamizi wa taka (Better waste management)
Kaulimbiu iliyotolewa kwa mwaka
huu, pia inahimiza nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutumia ngazi zote
za Serikali pamoja na wadau wote muhimu kutafakari nanma ya kuibua
mikakati ya kuwezesha uwepo wa nyumba bora na za gharama nafuu katika
nchi zao ikiwa ni utekelezaji wa mojawapo ya Agenda Mpya ya Makazi
Duniani iliyoidhinishwa Quito, Oktoba, 2016 na Malengo Endelevu ya
Milenia.
Chimbuko la maadhimisho hayo ni
Azimio Namba 40/202 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa
mwezi Desemba mwaka 1985 na kuanza kuadhimishwa rasmi mwaka 1986.
No comments:
Post a Comment