Thursday 12 October 2017

WIZARA ya Mambo ya Ndani kuanza kukagua magari ya abiria nchini

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imetangaza kuanza ukaguzi mkali kwa magari ya abiria, wanafunzi na mizigo huku yale yatakayokutwa salama ndiyo yatakayopewa stika za usalama barabarani.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni, alitangaza ukaguzi huo jana na kueleza kuwa utaanza kufanyika wakati wa wiki ya
‘nenda kwa usalama barabarani’ inayotarajia kuanza Jumatatu ijayo.

Masauni alisema wanataka kuyaondoa magari mabovu barabarani kwa sababu Tanzania sio sehemu yake.

Aidha, waziri huyo alisema kila mwaka kikosi cha usalama barabarani kupitia wiki ya nenda kwa usalama barabarani, kimekuwa kikitoa stika hizo, lakini utolewaji umeonekana kufanyika kiholela.

Alisema wapo baadhi ya askari waliokuwa wakitoa stika hizo kiholela na walipobainika walichukuliwa hatua zikiwamo kufukuzwa kazi na kushtakiwa kijeshi.

“Tunataka kukomesha jambo hili, ili gari lipewe stika litakaguliwa na wataalamu watakapojiridhisha lipo salama ndipo litapewa stika, kuendelea kwa ajali ni dhahiri kuwa yapo magari mabovu barabarani,” alisema.

Masauni alisema vipo vyanzo mbalimbali vya ajali za barabarani zikiwamo zile za makosa ya kibinadamu ambazo zipo kwa asilimia 70 na makosa mengine ni ya vyombo vya usafiri kuwa vibovu na pia changamoto za miundombinu.

“Kwa makosa ya vyombo vya usafiri, mfano ni ajali ya Hiace iliyosababisha vifo Mwanza baada ya kuingia ziwani. Tunataka kupunguza au kuzikomesha kabisa ajali za namna hii. Kwa hiyo hakuna stika itakayotolewa bila chombo cha usafiri kukaguliwa,” alisema.

Alisema tathmini ya ukaguzi huo wa magari ya abiria, wanafunzi na mizigo ndio itakayowezesha kwenda kwenye awamu ya pili ya ukaguzi wa magari ya watu binafsi.

“Ukaguzi wa magari ya watu binafsi kwa sasa tumesitisha hadi tujiridhishe kwenye ukaguzi wa vyombo hivi vingine. Ukaguzi huu utashirikisha taasisi mbalimbali ikiwamo Taasisi ya Usafirishaji ya Taifa (NIT) na Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA),” alisema.

Alisema yeyote atakayeendesha gari bovu hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

“Tunataka ukaguzi huu hapo baadaye ufanywe kwa teknolojia za kisasa. Mchakato wa kufikia huko unaendelea, kwa zoezi la sasa tutatumia rasilimali tulizonazo,” alisema.

Kadhalika, Masauni alisema sheria ya usalama barabarani ina upungufu na mchakato wa kuirekebisha unaendelea kabla muswada kufikishwa bungeni pindi utakapokamilika.

Masauni alitaja baadhi ya upungufu uliyopo kwenye sheria ya sasa kuwa ni pamoja na baadhi ya makosa kutoainishwa na mengine kuwa na adhabu ndogo zisizoendana na uzito wa makosa husika.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri anayeshughulikia masuala ya Ujenzi, kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, alisema katika kutatua changamoto ya miundombinu, wizara yake inatekeleza miradi ya ujenzi wa barabara mbalimbali zikiwamo za jijini Dar es Salaam.

Mhandisi Nditiye ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani, alisema Novemba mwaka jana hadi Agosti mwaka huu, zipo barabara ambazo zimejengwa na nyingine zikiendelea kujengwa.

“Barabara 24 zimekamilika, nyingine 32 zinatarajia kukamilika na lengo ni kuondokana na changamoto ya miundombinu ambayo nayo inatajwa kuwa ni chanzo cha ajali za barabarani,” alisema.

Katika mkutano huo, wizara hiyo ilitoa vyeti kwa makundi mbalimbali wakiwamo wasanii wa uigizaji likiwamo kundi la uchekeshaji la Mizengwe linalorusha vipindi vyake katika kituo cha televisheni cha ITV.

No comments: