Wednesday, 22 April 2015

KAMATI ZA KUDUMU ZA BUNGE KUKUTANA 26 APRILI HADI 9 MEI, 2015

index
Kamati za Kudumu za Bunge zitaanza kukutana tarehe 27 Aprili hadi tarehe 4 Mei 2015 Jijini Dar es Salaam, kutekeleza Majukumu yake, kabla ya Mkutano wa Bunge wa Bajeti uliopangwa kuanza mjini Dodoma tarehe 12 Mei na kudumu hadi tarehe 25 Juni, 2015. Kwa kawaida, Kamati za Kudumu za Bunge hupaswa hukutana wiki mbili kabla ya Mkutano wa Bunge, ama Dar es Salaam, Dodoma au Zanzibar kuendana na matakwa ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Aprili 2013.
Hivyo, Wabunge wote wanapaswa kuwa wamewasili jijini Dar es Salaam ifikapo Jumapili tarehe 26 Aprili 2015 tayari kwa kuanza vikao siku ya Jumatatu tarehe 27 Aprili, 2015.
2.0 SHUGHULI ZITAKAZOTEKELEZWA
katika vikao hivyo Kamati 13 za Bunge zitajadili utekelezaji wa Bajeti ya Serikali katika ngazi ya Wizara, Idara na Taasisi kwa mwaka 2014/2015 na mapendekezo ya mapato na matumizi kwa mwaka 2015/2016.
Siku ya Jumatano tarehe 28 Aprili, 2015 Wabunge wote kwa ujumla wao watakutana katika Ukumbi wa Julius Kambarage Nyerere kupokea Mapendekezo ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti ya Serikali ya 2015/2016 kwa mujibu ya matakwa ya Kanuni ya 97 ya kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la 2013. Baada ya shughuli hiyo, Kamati zote za Kisekta zitaendelea na uchambuzi wa Bajeti kuanzia tarehe 29 Aprili hadi 8 Mei, 2015.
Pamoja na hayo, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali itatumia muda huo kujadili Hesabu za Mikoa zilizokaguliwa zinazoishia tarehe 30 Juni, 2013 na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa itafanya ziara za ukaguzi wa thamani kwa miradi ya maendeleo iliyotekelezwa kwa mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2013 katika mikoa ya Dodoma na Singida.
Tofauti na kamati nyingine, Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imeanza kazi zake mapema tarehe 20 Aprili, 2015 ambapo inajadili Bajeti za Mikoa ya Tanzania Bara na Bajeti ya Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mwaka 2015/2016.
3.0 SHUGHULI NYINGINE
Shughuli za Kamati zitamalizika tarehe 8 Mei, 2015 Jijini Dar es Salaam ambapo Mkutano wa Bunge wa Bajeti utaanza tarehe 12 Mei, 2015 Mjini Dodoma na unategemewa kumalizika tarehe 25Juni, 2015. Ratiba za shughuli za Kamati zote zitapatikana kwenye tovuti ya Bunge ambayo ni www.parliament.go.tz
Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa,
Ofisi ya Bunge
DAR ES SALAAM
22 Aprili 2015

No comments: