Abiria wakigombania kuingia ndani ya daladala. Pamoja na shida hii lakini Sumatra imeshindwa kushusha nauli.
MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imetangaza kushusha nauli za mabasi ya Masafa Marefu huku ikiacha kabisa kuzigusa nauli za mabasi katika miji mikubwa, maarufu kama daladala.
Viwango hivyo vipya vya nauli vitaanza kutumika Aprili 30 mwaka huu, na mabasi yote ya mikoani yataandikwa daraja la basi ili wananchi watozwe nauli kulingana na daraja lake.
Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliad Ngewe alisema hayo jana wakati akitangaza hatua iliyofikiwa na bodi ya Mamlaka hiyo kuhusu kushuka kwa nauli za masafa Marefu na mijini.
Pia wameunda daraja jipya la Kawaida Juu kuwa Sh 44.96 huku Daraja la kati kuwa Sh 50.13 kwa kilometa kutoka Sh.53.22 na kuamua nauli za mabasi ya hadhi ya juu kutodhibitiwa ili kuchochea ubunifu katika utoaji huduma na ushindani kwa mabasi hayo ambayo hayazidi 10 nchi nzima.
Alitaja baadhi ya mikoa na nauli zilivyoshuka kuwa ni kutoka Dar es Salaam hadi Arusha kwa Daraja la kawaida la chini itakuwa Sh 21,000 badala ya Sh 22,700 huku Daraja la kati ikiwaSh 31,000 badala ya Sh 32,800 ambapo daraja jipya la kawaida la juu itakuwa Sh 28,000.
Kuelekea mkoa wa Dodoma kutoka Dar es Salaam kwa Daraja la kawaida la chini itakuwa 15,500 badala ya Sh 16,700 na Daraja jipya la kawaida la juu itakuwa Sh 20,500 na daraja la kati itakuwa Sh 23,000 badala ya Sh 24,100.
Mkoani Mwanza kwa daraja la kawaida la chini itakuwa Sh 39,500 badala ya Sh 42,600 daraja jipya la kawaida la juu Sh 52,000 na Daraja la kati itakuwa Sh 58,000 badala ya Sh 61,400.
Ngewe alisema Machi 9 mwaka huu, Baraza la Ushauri la watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Sumatra CCC, waliwasilisha maombi ya kutaka kushuka kwa nauli hizo kwa sababu bei ya mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya imeshuka kutoka asilimia 25 hadi 10.
Alisema baada ya mamlaka hiyo kupitia taratibu zote za kuwashirikisha wadau na baadaye bodi kukataa na kutafakari kwa kina walibaini kuwa ni kweli bei ya mafuta imeshuka kutoka bei ya awali ya ukomo mwaka 2013 ambapo dizeli ilikuwa Sh 2071.67 lakini kufikia Machi mwaka huu ilikuwa sh 1665.38 na mwezi huu Sh 1,779.57.
Pia ilibaini kuwa mwenendo wa bei hiyo umekuwa ukibadilika na kwamba kulikuwa na uwezekano wa bei kupanda, lakini gharama ya mafuta inachangia kwa asilimia 30 tu ya uendeshaji wa vyombo hivyo.
Akizungumzia punguzo la ushuru wa forodha kwa uingizaji wa mabasi mapya, alisema lilikuwa na athari chanya kuchochea uingizaji wa mabasi mapya nchini hata hivyo sehemu kubwa ya mabasi yaliyopo hayakupata punguzo kwani yaliingizwa kabla ya punguzo. Alisema ni mabasi 373 pekee yaliyopata nafuu hiyo kati ya 35,000 yenye leseni nchini.
Alisema udhibiti wa nauli unafanyika kwa madaraja matatu ili kutimiza wajibu wa kuwalinda watumiaji wenye kipato cha chini. "Ninawaagiza wamiliki wa mabasi na wafanyakazi wao kutoza viwango vya nauli vilivyoidhinishwa na Mamlaka na wananchi nawaasa kuwasiliana na mamlaka wanapotozwa nauli za juu tofauti na hizi,"alisema.
Akizungumzia nauli za mijini,Ngewe alisema ni kweli bei ya mafuta ilishuka kwa wastani wa bei ya lita ya dizeli mwaka 2013 lita ilikuwa Sh 2071.67 kufikia machi bei ilikuwa Sh 1,665.38 na mwezi huu Sh 1,779.57 ambapo mwenendo wa bei ya mafuta inabadilika na kuna uwezekano wa kupanda.
Alisema punguzo la ushuru wa magari ya mijini hayakupata punguzo kwani yaliingizwa kabla haijaanza na gharama za utoaji huduma za usafiri mijini zinapaswa kutazamwa kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja na punguzo la mafuta ili kupata viwango vya nauli vinavyostahili.CHANZO:HABARI LEO (Muro)
No comments:
Post a Comment