Tuesday 19 May 2015

Kipindupindu Chalipuka kwa wakimbizi wa Burundi Walioko Katika Kambi ya Kigoma.


WAKATI hali ya usalama nchini Burundi ikiwa bado tete, wakimbizi 558 walioko katika kambi ya Nyarugusu mkoani Kigoma wanaugua ugonjwa wa Kipindupindu.
 
Ugonjwa huo ulilipuka hivi karibuni baada ya wakimbizi hao kuingia nchini wakikimbia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.
 
Akizungumza jana, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Steven Kebwe, alisema hadi sasa wakimbizi 15 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
 
Alisema tangu Aprili 24 mwaka huu wakimbizi 2,458 walikuwa wakiharisha na kutapika na sampuli 11 kati ya 13 zilizochukuliwa juzi zilithibitisha kuwa wanaugua ugonjwa wa kipindupindu.
 
“Tumeshirikiana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) na tayari tumepeleka timu ya wataalamu ambao wametembelea maeneo ya Kagunga na Nyarugusu kutathmini na kutoa elimu ya afya kwa umma.
 
“Tumefanya tathmini katika mikoa ya Kagera, Geita na Katavi ambayo inapakana na Burundi,” alisema Dk. Kebwe.
 
Alisema wamepeleka dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya dharura pamoja na kuanzisha mfumo wa kufuatilia magonjwa yakiwemo ya mlipuko katika maeneo yaliyoathiriwa.
 
Kwa mujibu wa Dk. Kebwe, ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kula chakula au kunywa kinywaji chenye vimelea vinavyosababisha kuharisha ambavyo hupatikana kwenye kinyesi, matapishi au majimaji kutoka kwa mgonjwa.
 
Alizitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni kuharisha mfululizo bila maumivu ya tumbo, kinyesi cha majimaji kinachofanana na maji ya mchele, kutapika mfululizo, kuishiwa nguvu na kwamba ndani ya masaa sita kama hakuna huduma mgonjwa anaweza kupoteza maisha.
 
Kuhusu gharama za matibabu, alisema wametoa kwenye akiba ya magonjwa ya dharura na mlipuko lakini zitarejeshwa baadaye na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).
 
Alitoa wito kwa wananchi kuzingatia usafi wa mazingira, usafi wa vyoo, kunywa maji safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni kabla na baada ya kutoka chooni na kusafisha vyakula.

No comments: