Friday 30 September 2016

Taarifa Ya Kanusho Kuhusu Tangazo La Ajira Serikalini

Kuna tangazo ambalo linasambazwa kupitia baadhi ya mitandao ya kijamii lenye kichwa cha habari ‘’Sekretarieti ya Ajira yatangaza zaidi ya nafasi za kazi 1,000’’. Likionyesha kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma inawatangazia watanzania wenye sifa na uwezo kujaza jumla ya nafasi wazi za kazi 1,101 kwa niaba ya waajiri mbalimbali Serikalini.

Katibu wa Sekretarieti ya Ajira anapenda kuwataafu wadau na wananchi wote kwa ujumla kuwa taarifa hiyo haina ukweli wowote na inalenga kuupotosha Umma, hivyo wananchi wote wanapaswa kuzipuuza. 

Matangazo yote ambayo hutolewa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni lazima yaonekane kwenye Tovuti ya Sekretarieti ya Ajira www.ajira.go.tzau portal ya Ajira ambayo niportal.ajira.go.tz.

Kama mnavyofahamu hivi karibuni Serikali ilitoa taarifa ya kusitisha Ajira mpya Serikalini kwa ajili ya zoezi la uhakiki wa Watumishi hewa kama ambavyo taarifa ilivyotolewa hapo awali, kwa kuwa zoezi hilo bado halijakamilika tunaomba wananchi wote na wadau wa Sekretarieti ya Ajira waendelee kuvuta subira hadi pale zoezi hilo litakapokamilika na taarifa rasmi itatolewa na Mamlaka husika.

Sekretarieti ya Ajira inapenda kuomba radhi kwa wale wote waliopata usumbufu kutokana na tangazo hilo lenye nia ya kupotosha Umma. 

Aidha,tunaendelea kuwasisitiza wadau wetu wote kuwa, wanapoona matangazo ya kazi yanayodaiwa kutolewa na Sekretarieti ya Ajira katika baadhi ya mitandao ya kijamii wasiyokuwa na uhakika nayo wajiridhishe kwa kuangalia katika tovuti na portal ya Sekretarieti ya Ajira kabla ya kuyafanyia kazi.

Aidha, Sekretarieti ya Ajira inapenda kutoa taarifa kuwa haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wenye nia ya kuupotosha umma kupitia taarifa zinazosambazwa ambazo hazina ukweli.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Tarehe 30 Septemba, 2016

No comments: