Friday 29 September 2017

Aliyeandika Whatsap Taarifa za Uongo Kuhusu Polisi Kuonekana Hospitali kwa Tundu Lissu Afikishwa Mahakamani


SeeBait
Mtu mmoja wa Kigamboni, amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kusambaza ujumbe katika mtandao kwamba kachero wa Usalama wa Taifa ameonekana jijini Nairobi karibu na hospitali aliyolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Mshtakiwa huyo Mbutusyo Mwakihaba (40), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  na kusomewa shtaka linalomkabili mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.

Wakili wa Serikali Janeth Magoho alidai mshtakiwa anakabiliwa na kosa la kusambaza taarifa za uongo chini ya kifungu namba 16 cha Sheria ya mtandao namba 4 ya mwaka 2015.

Janeth amedai Septemba 11, mwaka huu kupitia mtandao wa ‘WhatsApp’ mshtakiwa aliandika “Huyu ni Kachero wa Usalama wa Taifa anatambulika kwa jina la Jose anaonekana Nairobi karibu na hospitali alikolazwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu…Mwaxcheni mwenzenu”.

Mshtakiwa alikana kutenda makosa hayo, upelelezi wa kesi haujakamilika ambapo Hakimu Nongwa alikubali kumpa dhamana kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini dhamana ya Sh milioni tano kila mmoja ambapo mshtakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo na kurudishwa mahabusu hadi Oktoba 12, mwaka huu.

No comments: