Suala
la Meya wa Ubungo, Boniface Jacob na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda, limechukua sura mpya baada ya meya huyo kuitwa
Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma na kutakiwa kujibu shauri
lililofunguliwa la matumizi ya ofisi ya umma kwa shughuli za chama
chake.
Machi
22, mwaka huu Meya Jacob aliwasilisha mashitaka dhidi ya Makonda kwa
Sekretarieti hiyo, akitaka achukuliwe hatua za nidhamu kwa kukiuka
maadili ya utumishi wa umma kwa kutumia vyeti feki na hivyo kukosa sifa
ya kuwa kiongozi.
Akizungumza
na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kutoka katika mahojiano na
sekretarieti hiyo jana, Jacob alisema sekretarieti hiyo imemwomba
kujibu shauri hilo ikisema kwa kuwa hata yeye aliwahi kutumia Ofisi za
Manispaa ya Ubungo kwa vikao vya chama chake.
“Wameniomba
kuondoa shauri hili kwa madai kuwa walipomwita Makonda alisema
tuyamalize kwa kuwa hata mimi nilitumia ofisi ya umma kufanya vikao vya
chama… mimi nimesema ruksa kunihukumu kama wana ushahidi wa kutosha,”
alisema Jacob.
Alisema
uhalali wa Makonda kumhoji kuhusu kufanya vikao vya chama katika ofisi
ua umma ndiyo mwanzo wa uhalali wa kumhoji mkuu wa nchi uhalali wa
kufanya vikao vya chama Ikulu.
“Hakuna
kikao ambacho nilikiongoza mimi nikiwa na wafuasi wa chama, ninachojua
nilitembelewa na Frederick Sumaye. Kiongozi wa Chadema akinitembelea
nimkatae? “Lakini wenzetu wamefika mbali kwa kuvaa sare za chama na
kuzungumza masuala ya chama,” alisema.
Alisema
wanaporuhusu mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kumuuliza kuhusu hilo
walipaswa waanze kujitafakari kuwa kuna Halmashauri ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) inafanyika Ikulu.
Alisema walimwambia hakuna mtu aliyewahi kulalamika kwa nini mikutano ya CCM inafanyika Ikulu.
“Sheria inasema wao waliposikia tu kuwa Makonda ana vyeti feki walitakiwa kumwita na si kusubiri mtu aende kushtaki.
“Wao
kama wasimamizi wa maadili ya umma wakiona mtu anarudisha fedha za
rushwa benki hawakustahili kusubiri mtu wa Chadema kwenda kushtaki,”
alisema Jacob.
Jacob alisema alipewa dakika 10 za kuandika malalamiko kwa nini CCM inafanyia vikao vyake Ikulu.
“Nimewakabidhi ushahidi wa picha na video za vikao vya Chama cha Mapinduzi Ikulu,” alisema Jacob.
Alisema
lengo lake si kulalamika kuwa CCM inafanyia vikao vyake ikulu bali
suala la vyeti feki ambalo anahitaji lifikishwe katika Baraza la
Maadili.
No comments:
Post a Comment