Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani amemtaka Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk Tito
Mwinuka kuandika barua kujieleza ni kwa nini ameshindwa kuanza ujenzi wa
kituo cha kupoozea umeme cha Kigamboni.
Dk Kalemani ametoa agizo hilo baada ya kutembelea vituo vya kupoozea umeme vya Gongo la Mboto, Kurasini na Kigamboni.
Mwezi
uliopita naibu waziri alimwagiza Dk Mwinuka kuanza ujenzi haraka lakini
baada ya kutembelea jana Jumatatu amekuta eneo hilo bado halijafanyiwa
usafi.
“Nataka
kesho( leo) nipate taarifa ya maandishi ni kwa nini hadi sasa hujaanza
ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Kigamboni licha ya kukuagiza
uanze ujenzi,” aliagiza.
Dk Kalemani alisema Agosti alitembelea eneo hilo na kumuagiza mkurugenzi kujenga uzio ili watu wasivamie eneo hilo.
Alisema pia, alimuagiza kuanza ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme kwa sababu Sh5 bilioni zimeshatengwa kwa kazi hiyo.
“Nashangaa
sasa ni mwezi mmoja lakini hakuna kilichofanyika, umeshindwa hata
kufyeka majani ili kuonyesha kuna mradi utafanyika hapa,” alihoji Dk
Kalemani.
Naibu
waziri aliagiza makandarasi kwenye vituo vya kupoozea umeme kumaliza
kazi kwa wakati ili kuondoa matatizo ya umeme kwa wakazi wa Mbagala,
Kigamboni na Gongo la Mboto.
“Sitalala nitakuwa natembelea miradi hii kila mara hadi itakapokamilika,” alisema.
Akizungumzia
agizo hilo, Dk Mwinuka alisema tangu naibu waziri alipolitoa wamekuwa
wakifuatilia kibali cha athari za mazingira ambacho hutolewa na Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc).
“Tukipata kibali tutaanza ujenzi mara moja na tunakuahidi kazi hiyo itamalizika kwa muda uliopangwa Machi mwakani.
Mbunge
wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile alisema kuchelewa kukamilika kwa
vituo vya kupoozea na kusambaza umeme kunasababisha matatizo ya nishati
isiyo ya uhakika katika jimbo hilo.
Mkuu
wa Wilaya ya Kigamboni, Hashim Mgandilwa alisema mradi huo ukianza
atausimamia kwa kuwa tatizo la umeme linaathiri maendeleo na uchumi.
“Kila
siku napokea ujumbe wa maandishi wa simu kunijulisha tatizo la umeme,
ni aibu kwa kuwa wakati mwingine nashindwa nijibu nini,” alisema.
No comments:
Post a Comment