Serikali
kupitia kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
imekanusha madai yaliyotolewa na Aliko Dangote kuwa, sera za serikali ya
awamu ya tano chini ya Rais Dkt Magufuli zinatishia wawekezaji.
Akizungumza
na gazeti la The Citizen jana, Waziri Mwijage amesema kuwa sera za
uwekezaji ziko wazi na zina lenga kuhakikisha kuwa, serikali pia
inanufaika na rasilimali za nchi.
Dangote
ambaye ni tajiri namba moja Afrika alinukuliwa akisema kuwa, serikali
imeweka sera ambazo zinaifanya imiliki asilimia kubwa ya hisa kwenye
mali.
"Wanawatisha
wawekezaji wengi, na kuwatisha wawekezaji sio kitu kizuri kufanya,"
alisema Dangote katika mkutano wa Afrika uliofanyika jijini London.
Dangote
ni miongoni mwa wawekezaji Tanzania ambapo anamiliki kiwanda cha saruji
chenye thamani ya Tsh 1.3 trilioni katika Mkoa wa Mtwara.
Waziri
Mwijage alisema kuwa, wawekezaji katika Sekta ya Uchimbaji wanatakiwa
kutoa umiliki wa asiliimia 16 kwa serikali ili kuhakikisha kuwa nchi
inafaidika kutokana na rasilimali zake. Aliongeza waziri huyo kwamba,
anategemea mtu kama Dangote ambaye ni mwekezaji mkubwa nchini, awe na
uelewa kuhusu sheria za nchi.
"Kampuni
inapokuja kuwekeza katika sekta ya uchimbaji, hisa za serikali
hazitakiwi kuwa chini ya asilimia 16, na hili si kosa kabisa kwa sababu
rasilimali ni zetu," alisema Waziri Mwijage.
Aidha,
Waziri Mwijage alisisitiza kuwa atahakikisha wawekezaji wote nchini
wanafuata sheria, na kwamba hakutegemea kama Dangote angekuwa mmoja wa
watu ambao wangekosoa mazingira ya uwekezaji Tanzania.
“Dangote
amekuwa hana tatizo hapa. Wakati wowote anapokumbwa na tatizo, serikali
yote hukimbia na kumsaidia. Unakumbuka alipokuwa na tatizo mwaka jana,
wote tulikuwepo kwa ajili ya kumsaidia,” alisema Waziri Mwijage.
Katika
mkutano huo, Dangote alisema uhusiano wake na Rais Magufuli ni mzuri,
lakini akamshauri kuangalia upya sera zake za uwekezaji.
No comments:
Post a Comment