Thursday 23 April 2015

Mwili wa mwanafunzi Kiteto Aliyefariki Kwa Kuchapwa Viboko na Walimu wafikishwa Dodoma



MWILI wa mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari Matui iliyoko Wilaya ya Kiteto, Mkoa wa Manyara, aliyedaiwa kufariki baada ya kuchapwa viboko na walimu wake, Emmanuel Mbigima (15), umefikishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Wakati mwili huo unafikishwa hospitalini hapo jana asubuhi, ulikuwa umewekwa kwenye gari la Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto ukisindikizwa na baadhi ya ndugu wa karibu wa familia ya marehemu.

Akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo, babu wa marehemu, Emmanuel Ngowi, alisema mwili huo umeletwa hospitalini hapo kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ambavyo vimekosekana katika hospitali ya Wilaya ya Kiteto.

"Mjukuu wangu alipigwa na walimu watatu tarehe 20 mwezi huu kutokana na kufeli mtihani wa somo la Kiswahili.

“Tumechukua uamuzi wa kumleta hapa kwa sababu madaktari wa Hospitali ya Wilaya ya Kiteto, walishindwa kubaini kichwa kimeathirika kwa kiasi gani kwa kuwa hawana vifaa vya uchunguzi vya  kichwa.

“Hata hivyo, majibu ya uchunguzi wa awali yaliyotolewa katika hospitali hiyo, yalionyesha jicho la kulia lilivuja damu kwa ndani na pia mwili wa marehemu ulikuwa na michubuko miguuni,” alisema Ngowi.

Naye mjomba wa marehemu, Michael Ezekiel alisema matukio ya wanafunzi kupigwa na kupoteza maisha yamekuwa yakijirudia shuleni hapo kwa kuwa hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

“Mwaka jana kuna mtoto alipigwa na mwalimu akafariki, lakini mtuhumiwa alipelekwa mahakamani na baadaye kuachiwa kwa madai kuwa mtoto alikuwa ni mgonjwa,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk. Zainabu Chaula, alithibitisha kupokelewa kwa mwili huo na kusema uchunguzi bado unaendelea.

No comments: