Thursday 23 April 2015

WANAJESHI WA RWANDA WADAIWA KUINGIA DRC

Wanajeshi wa DRC wakipiga doria
Msemaji wa Serikali ya DRC amesema kuwa wanajeshi wa Rwanda wameonekana nchini humo katika hifadhi ya Wanyama ya Virunga, Kilomita 120, Kaskazini mwa Goma, mji mkuu katika mkoa wa Kivu Kaskazini.
Lambert Mende anasema kuwa majeshi ya DRC yalifyatua risasi za kutoa onyo, ambapo wanajeshi wa Rwanda nao walijibu kwa risasi na kumjeruhi mwanajeshi mmoja Mkongomani.
Msemaji wa Serikali anasema kuwa majeshi ya kigeni yote kisha yalitorokea Rwanda.
Lakini afisa mmoja katika Hifadhi ya wanyama ya Virunga aliiambia BBC kuwa wanajeshi 300 wa Rwanda wanadhaniwa kuwa walivuka mpaka na kuwa wengi wao huenda walitorokea msituni.
Kisa hicho kilikanushwa kupitia mtandao wa Twitter na naibu mwakilishi wa Rwanda katika Umoja wa Mataifa, aliyesema kuwa madai hayo ni upuzi mtupu.
Rwanda imekosoa Serikali ya DRC na Ubalozi wa Umoja wa Mataifa nchini kwa kukosa kushughulikia kikamilfu maswala yanayohusu kundi la waasi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda, kundi la waasi kutoka Kabila la Wahutu ambalo limekuwa katika Congo kwa zaidi ya miaka 20.
Mara kadhaa siku zilizopita Rwanda imewahi kuyatuma majeshi yake kukabiliana na waasi nchini DRC.

No comments: