Friday 5 May 2017

Mavazi Yaibua Mjadala Bungeni.....Naibu Waziri Ajibu Madai ya Wanawake Kuvuliwa Hijabu na Polisi

Naibu Waziri, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akiwa bungeni leo amefunguka na kusema hakuna tafsiri ya mavazi ya kike au kiume kwa kuwa mavazi hayo kama suruali yanavaliwa na watu wote wanaume hata wanawake.

Masauni alitoa ufafanuzi huo bungeni kufuatia Mbunge kutaka kujua serikali inachukua hatua gani kwa baadhi ya wanaume ambao wamekuwa wakijipamba na kujilemba kwa kuvaa nguo za kike.

"Ni kweli kuna wanaume wanavaa mavazi ya kike hata wanawake pia wapo wanavaa mavazi ya kiume, ila sidhani suala la mavazi kama lina tafsiri kuwa vazi hili ni la kike tu na hili ni la kiume tu, nadhani suala hili la Mbunge linahitaji ufafanuzi wake wa kina ili tujue yeye alikuwa anamaanisha nini zaidi katika jambo hili" alisema Masauni

Mbali na hilo Naibu Waziri huyo alitolea ufafanuzi malalamiko ambayo yametolewa kuwa wapo baadhi ya wanawake huvuliwa hijabu zao na kusema si kweli kwani polisi wanafanya kazi zao kwa weledi na kufuata sheria.

"Si kweli kwamba wanawake wanavuliwa hijjabu na nikabu zao na polisi wa kiume pindi wanapokaguliwa kwani polisi wanafanya kazi zao kwa kufuata sheria na umakini mkubwa, ila kama wapo watu wanafanya hivyo niwaombe wanawake wote pindi wanapofanyiwa hivyo wapeleke malalamiko yao kwenye vyombo husika tutalifanyia kazi, natambua kule Zanzibar kuna changamoto katika kufanya ukaguzi lakini hatukuona wanawake wakivuliwa mavazi yao" alisisitiza Masauni

No comments: